Alhamisi 12 Novemba 2026 - 12:30
Serikali ya Lebanon Yashindwa Katika Jaribio Lake la Kwanza; Jopo la Wanazuoni wa Beirut Lakosoa Vikali Utegemezi wa Nje

Hawza/ Jopo la Wanazuoni wa Beirut, kupitia taarifa rasmi, limelaani uingiliaji wa wazi wa mataifa ya kigeni katika masuala ya ndani ya Lebanon na kuilaumu mamlaka ya nchi hiyo kwa hali iliyopo sasa.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Jopo la Wanazuoni wa Beirut, katika taarifa rasmi, limelaani uingiliaji wa wazi wa mataifa ya kigeni katika masuala ya Lebanon na kuitaja mamlaka ya nchi hiyo kuwa ndiyo inayowajibika kwa hali iliyopo.

Jopo hilo, likilinganisha hali ya sasa na kipindi cha «Utawala wa Makonsuli», limeeleza kuwa Lebanon, chini ya mazingira ya utawala na udhibiti wa kigeni, imegeuzwa kuwa uwanja wa uingiliaji wa nje na ukiukaji wa mamlaka yake ya kitaifa, hata katika masuala madogo kabisa ya ndani. Hali hiyo imesababisha kusambaratika taasisi za kikatiba nchini humo.

Kukosoa ukimya wa mamlaka ya Lebanon mbele ya uingiliaji wa mataifa ya kigeni

Katika taarifa yake, Jopo la Wanazuoni wa Beirut limesema kuwa «vitendo vya aibu na vya kutisha» vinavyoendelea kushuhudiwa vilipaswa kukabiliwa kwa upinzani na kulaaniwa. Hata hivyo, hali iliyopo sasa inaonesha ukimya wa taasisi zinazojinasibu kwa kaulimbiu za kulinda mamlaka na uhuru wa kitaifa.

Jopo hilo, likilaani uingiliaji wa mataifa ya kigeni, hususan taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na balozi tano kuhusu masuala ya ndani ya Lebanon, limesisitiza kuwa; balozi hizo hazina haki ya kuingilia wala kutoa maoni kuhusu masuala hayo.

Wito kwa balozi za kigeni: Iungeni mkono Lebanon badala ya kuingilia masuala yake ya ndani

Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa; ikiwa balozi hizo zina wasiwasi wa kweli kuhusu Lebanon, utulivu wake na kulindwa kwa mamlaka yake ya kitaifa, basi ilipaswa zichukue msimamo thabiti dhidi ya mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel kusini mwa Lebanon.

Mashambulizi hayo yanaendelea usiku na mchana mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa, sambamba na kuingia mamia ya malori yanayobeba vifaa vya vilipuzi na uharibifu wa kikatili wa makumi ya vijiji.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa; wajibu hauwahusu wahusika wa moja kwa moja wa mashambulizi hayo pekee, bali pia unayahusu makundi yanayowaunga mkono pamoja na wale wanaokaa kimya mbele ya jinai zinazofanyika kila siku dhidi ya Lebanon na mamlaka yake ya kitaifa.

Udhaifu na kushirikiana Serekali ya Lebanon na adui mbele ya uchokozi

Jopo la Wanazuoni wa Beirut, likiweka maendeleo haya mbele ya mamlaka ya Lebanon, limesema kuwa; serikali ina jukumu la kulinda mipaka ya nchi, lakini kiutendaji imejionesha kuwa dhaifu, imeshindwa kutekeleza wajibu wake na kushirikiana na upande wa adui.

Kwa mujibu wa jopo hilo, utegemezi wa mamlaka ya Lebanon kwa mataifa ya kigeni umefungua milango ya aina mbalimbali za uingiliaji wa nje, kuchezea sheria na kuendelea kwa mashambulizi. Hali hiyo imewafanya wakaliaji wa ardhi ya Lebanon kuepuka kuwajibishwa kwa uharibifu na mashambulizi wanayoyafanya dhidi ya maeneo ya kusini mwa nchi hiyo na wakazi wake.

Katika upande mwengine Jopo hilo pia limekosoa hatua za mamlaka ya Lebanon za kutoa masharti na makubaliano ya upendeleo kwa adui bila kupata matokeo yoyote chanya. Limebainisha kuwa wakaliaji hao hawakuridhika na yale ambayo tayari wamepewa, bali wanaendelea kudai kupewa masharti na upendeleo zaidi.

Jopo la Wanazuoni wa Beirut limeitaja mamlaka ya Lebanon kuwa ndiyo inayowajibika kikamilifu kwa yote yanayoendelea nchini humo, likisema kuwa serikali imeshindwa katika jaribio lake la kwanza wakati wa mashambulizi ya hivi karibuni.

Mwisho wa taarifa hiyo, jopo hilo limesisitiza haki ya kufanya Muqawama dhidi ya uvamizi na kupigania ukombozi wa ardhi. Limeeleza kuwa haki hiyo imehakikishwa na Katiba, sheria za kimataifa pamoja na sheria za Mwenyezi Mungu zilizoteremshwa kupitia dini za mbinguni.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha